Breaking

Tuesday 13 June 2023

MUUGUZI ATUHUMIWA KUMBAKA MJAMZITO



 

Na Lucas Raphael,Tabora

 

MUUGUZI wa hospitali ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa kwa tuhuma za kubaka mama mjamzito aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.

 Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo na kubainisha mtumishi aliyehusika na tukio kuwa ni Afisa Muuguzi Msaidizi (ANO) Rayson Agnelus Duwe.

Alisema mjamzito huyo alifikishwa hospitalini hapo Juni 9 mwaka huu majira ya saa 2 usiku akiwa anasumbuliwa na malaria ambapo alilazwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu zaidi.

Alibainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonesha Mtumishi huyo aliyekuwa zamu siku hiyo alikuwa eneo la mapokezi ya wagonjwa wa nje (OPD) na aliingia kazini akiwa amelewa.

Kamanda alifafanua kuwa mtuhumiwa akiwa na jukumu la kupokea wagonjwa (mapokezi) alitoka na kwenda chumba cha mgonjwa huyo na kumfanyia kitendo hicho.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa alikutwa na wenzake akiwa chumbani humo na pembeni yake kulikuwa na vifaa vilivyotumika kumchoma mhanga dawa ya usingizi ijulikanayo kwa jina la diazepam injection ambayo ilimfanya mama huyo kupata usingizi hivyo kumbaka.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo tayari umekamilika na mtuhumiwa amepandishwa kizimbani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa wilaya hiyo ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya Simon Chacha alisema hatua ya awali waliyochukua ni kumsimamisha kazi huku jeshi la polisi likiendelea na kazi yake.

Aliwataka watumishi wa umma wote katika halmashauri ya wilaya hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na kwa mujibu wa viapo vya taaluma zao na kuonya kuwa yeyote atakayekiuka maadili ya kazi yake hawatasita kuchukua hatua.

Mwisho.   

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages