Breaking

Wednesday 14 February 2024

MRADI WA LTIP KUWAPA NAFASI MAKAMPUNI WAZAWA YA UPANGAJI NA UPIMAJI

Na Magreth Lyimo MLHHSD

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi umedhamiria kuwapa nafasi makampuni ya upangaji na upimaji yanayomilikiwa na Watanzania nchini katika utekelezaji wa mradi kwenye maeneo ya urasimishaji mijini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upangaji na Upimaji kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Mazula Manyasa alipofungua mafunzo kwa makampuni ya upangaji na upimaji tarehe 14 Februari 2024, Jijini Dodoma yaliyoandaliwa na Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.

Utekelezaji wa kazi za mradi uko katika makundi mawili ambayo ni asilimia 20 inayoendelea kutekelezwa na watumishi wa Serikali pamoja na asilimia 80 ambayo inatarajiwa kutekelezwa na makampuni ya upangaji na upimaji yaliyopo nchini alisema Manyasa.

‘‘Wizara imeandaa mafunzo haya kwa makampuni ya upangaji na upimaji ili kujenga uelewa juu ya mradi na kazi mbalimbali zinazotegemea kufanyika ikiwa ni hatua muhimu kabla ya zoezi la manunuzi ambalo litalenga kuyashindanisha makampuni ya upangaji na upimaji na kupata makampuni yatakayoshiriki kazi za urasimishaji katika maeneo mbalimbali ya Mradi’’ alisema Manyasa

Bw. Manyasa alisisitiza kuwa ‘‘tumekutana hapa ili kubadilishana uzoefu pamoja na kukumbushana masuala yanayotakiwa yazingatiwe pamoja na Sheria mbalimbali za kuzingatia ili kutekeleza kazi zetu kwa weledi kwa yale makampuni yatakayofanikiwa katika mchakato wa manunuzi’’

Naye Meneja Urasimishaji kwa upande wa Mjini Bw. Leons Mwenda alisema kuwa kusudi la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya kazi mbalimbali za mradi na masuala muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa mradi hasa masuala ya kimazingira na kijamii ili kuwa na mtazamo mmoja pamoja na wananchi katika utekelezaji wa mradi.

‘‘Kwa kampuni zitakazopata nafasi katika utekelezaji wa mradi ni lazima wawe na afisa maendeleo ya jamii katika timu kwa kuwa Mradi umetoa kipaumbele cha kwanza kwa wananchi kuwa na uelewa wakutosha kuhusu mradi na manufaa yake’’ alisema Mwenda

Mradi unatarajia makampuni yatakayopata kazi hii kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi, kusaidia katika utatuzi wa migogoro, utoaji elimu na uhamasishaji katika ngazi ya Kata pamoja na Mitaa aliongezea Mwenda

Bw. Mwenda alisisitiza kuwa ''Suala la elimu na uhamasishaji kwa umma limepewa kipaumbele hivyo ni muhimu wadau wote kushiriki katika hamasa ili kuwa na uelewa wa pamoja na wananchi kwa kuzingatia makundi maalum kama wanawake, wazee, walemavu ili waweze kushiriki katika zoezi la urasimishaji''.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ni mradi unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa muda wa miaka mitano (2022-2027) ikiwa na lengo la kuongeza usalama wa milki za ardhi.
Kaimu Mkurugenzi wa Upangaji na Upimaji kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Mazula Manyasa akifungua mafunzo ya kujenga uelewa juu ya utekelezaji wa mradi wa LTIP kwa makampuni ya upangaji na upimaji tarehe 14 Februari 2024, Jijini Dodoma
Makampuni ya Upangaji na Upimaji wakiwa katika mafunzo juu ya shughuli mbalimbali zilizotekelezwa na mradi wa LTIP tarehe 14 Februari 2024, Jijini Dodoma
Mmoja wa washiriki katika mafunzo ya kujenga uelewa juu ya utekelezaji wa mradi wa LTIP yaliyofanyika tarehe 14 Februari 2024, Jijini Dodoma
Meneja Urasimishaji kwa upande wa Mjini Bw. Leons Mwenda akielezea utekelezaji wa mradi wa LTIP kwa washiriki kutoka kwenye makampuni ya upangaji na upimaji tarehe 14 Februari 2024, Jijini Dodoma
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages