Breaking

Thursday 5 September 2024

WANANCHI WA MIGANGA NA NKALAKALA WILAYANI MKALAMA WAHIMIZWA KUSHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Messos


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Messos amewataka wakazi wa kata za Nkalakala na Miganga wilayani Mkalama kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali Za Mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024.

Wito huo ameutoa Septemba 4,2024 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata hizo wilayani hapa.

“Mwaka huu tutakuwa na zoezi kubwa la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024, tujitokeze kwa wingi wetu tushiriki uchaguzi huu kwa maendeleo ya kata zetu. Usikubali mtu mwingine akuchagulie kiongozi wakati unauwezo wa kupiga kura” ,DED Asia Messos.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi.Asia Messos amesema kuwa ili mwananchi aweze kupiga kura siku ya Uchaguzi wa Serikali Za Mitaa, anapaswa kujiandikisja katika daftari la Orodha ya Wapiga Kura ambapo zoezi la uandikishaji litafanyika kuanzia Octoba 11-20,2024.

Aidha Bi. Asia Messos amewataka wanawake wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi huo kwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili waweze kushiriki katika maamuzi yatayoleta maendeleo ndani ya kata zao “Kina mama tujitokeze kwa wingi kuchukua fomu tuwe na viongozi wanawake kwenye nafasi za maamuzi” ,Bi. Asia Messos.

Akizungumzia kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Bi. Asia Messos amesema zoezi hilo kwa mkoa wa Singida linatarajia kufanyika Septemba 25,2024 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhuisha taarifa zao na ambao hawana kadi wajitokeze kwa wingi kujisajiri ili wapate kadi ya mpiga kura.

Awali akieleza mambo makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita katika miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bi. Asia Messos amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imepokea zaidi ya Bilioni 60 kwa ajili ya miradi mbalimbali kama vile elimu, afya, michezo, kilimo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages