Breaking

Tuesday 26 July 2022

WAZIRI DKT. BITEKO AMTAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI UJENZI WA MJI WA TANZANITE MIRERANI




Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la soko la madini ya Tanzanite lililopo katika Mji wa Tanzanite Mirerani uliopo wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara ambapo amemtaka mkandarasi wa zabuni hiyo kuongeza kasi ili mradi huo umalizike kwa wakati.

Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea ujenzi wa jengo hilo unaondelea katika Mji wa Tanzanite Mirerani wilayani Simanjiro ambao ulianza tarehe 22 Mei, 2022 na unatarajiwa kukamilika Mei, 2023 ambapo utaghalimu zaidi ya Tsh. bilioni 5.49.

“Haya ni maono aliyokuwa nayo Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuona mji huu unapata hadhi yake kama eneo ambalo Tanzanite inachimbwa, ukienda Geita utakuta mji huo umechangamshwa na dhahabu hivyo na Mirerani lazima inufaike na Tanzanite iliyopo katika eneo lake,” amesema Dkt. Biteko.

Awali, Dkt. Biteko alikutana na viongozi wa wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite, Mabroka, wafanyabiashara wakubwa wa Tanzanite (Dealers) na viongozi wa Eneo Tengefu la Mirerani ambapo aliwataka washiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusiana na maandalizi ya rasimu ya Kanuni za biashara ya Tanzanite.

Aidha, Dkt. Biteko amesema Mwaka wa Fedha 2021/22 Mchango wa Wachimbaji Wadogo wa Madini umeongezeka kufikia asilimia 44 kwenye Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 30 ya Mwaka wa Fedha 2020/21.


Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole-Sendeka amempongeza Dkt. Biteko kwa kuiongoza vyema Wizara ya Madini ambapo amemshukuru kwa kuendelea kuwashirikisha wadau wa madini kutoa maoni yao ili kuandaa rasimu ya Kanuni mpya za biashara ya Tanzanite.

“Udhibiti wa madini haya unakwenda vizuri lakini ombi langu ni kwamba, kituo cha utalii wa madini kijengwe Mirerani sababu Serikali imewekeza fedha nyingi hapa na isitoshe madini ya Tanzanite yanapatikana Mirerani pekee na ukizingatia uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA upo karibu na Mirerani,” amesema Sendeka.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mabroka nchini (CHAMMATA) Jeremiah Simon ametoa maoni yake kwa Dkt. Biteko ambapo ameshauri kwamba, Serikali iruhusu biashara ya madini ya Tanzanite yaliyoongezewa thamani ifanyike katika masoko ya madini ya hapa nchini ambapo kwa sasa Sheria ya Madini inasema biashara ya Tanzanite ifanyike Mirerani pekee.

“Madini ya Tanzanite hayaruhusiwi kutoka Mirerani kwenda kwenye masoko ya nje ya hapa, naomba zuio hili litolewe ili tuweze kuyatangaza madini yetu na pia, madini yakiongezewa thamani yaende kwenye masoko mbalimbali isiwe Mirerani pekee,” amesema Simon.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages