Breaking

Thursday 13 July 2023

WAFUNGWA WAFUNDISHWA KUSOMA NA KUANDIKANa Mwandishi Wetu

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini amepongeza hatua ya gereza la Igunga Mkoani Tabora kuanzisha programu ya kufundisha kusoma na kuandika kwa Wafungwa waliopo katika gereza ikiwa ni sehemu ya urekebu.

Sagini aliyasema hayo wakati alipotembelea katika gereza hilo kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika gereza hilo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la utawala pamoja na ngome ya gereza.

"Programu ya kutoa elimu kwa kuwafundisha Wafungwa kusoma na kuandika ni programu nzuri ambayo itawasadia kupata maarifa zaidi na kujua vitu muhimu ambavyo atakua amenufaika navyo pindi atokapo gerezani.

Niwapongeze pia kwa ubunifu mlioutumia wa kutumia rasilimali zilizopo ikiwa ni pamoja na Wafungwa katika kuhakikisha mnajenga ngome ya gereza hili hii ni hatua kubwa sana.Ni vyema Magereza ikaendelea kuwa na programu mbalimbali za urekebu ili mtu anapomaliza kifungo chake atoke na maarifa ambayo yatamsaidia kwenda kujiajiri na kuepukana na vishawishi vya kujiingiza katika kurudia makosa."

Kwa upande wake Inspekta Msaidizi Jeshi la Magereza Igunga Gilya Madede amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka sasa jumla ya Wafungwa 12 wasiojua kusoma na kuandika wamejiunga na darasa hilo na mpaka kufikia sasa wafungwa nane wameshajua kusoma na kuandika.

Madede ameongezea kuwa njia mbalimbali zimekuwa zikitumika kuwafundisha Wafungwa hao ikiwa ni pamoja na kuwatumia Wafungwa wanaojua kusoma na kuandika kuwafundisha na kuwasaidia wenzao mazoezi mbalimbali wanayopatiwa.

Baadhi ya Wafungwa ambao wameafanikiwa kushiriki katika darasa na shughuli za ujenzi wamesema kuwa hawakuwahi kuwaza kupata maarifa kutoka magereza lakini kwa sasa maarifa waliyoyapata na wanayoendelea kuyapata yatawasaidia katika kujitegemea na kuondoa ujinga pindi warudipo uraiani.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages